ATHARI ZA KUABUDU, KWENYE VITENDO NA MWENENDO

ATHARI ZA KUABUDU, KWENYE VITENDO NA MWENENDO


Kumpwekesha Allah kunadhihirika katika mwenendo wa mwanadamu na vitendo vyake. Kama ilivyo moyoni mwake, na ya kumcha Allah inadhihirika katika mwenendo wake pekee au yeye na wenzake, kwa hiyo uhai wote ni athari za imani na tawhiid na ibada. Amesema Allah Mtukufu:

{Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu} [Adh-dhariyat : 56]

Na miongoni mwa athari zake zilizo wazi katika mwenendo wa mwanadamu hasa:

Ya kwanza: athari khasa kwa mtu pekee:

TOHARA

Tawhiid [kumpwekesha Allah] ndilo jambo la pekee kubwa linaloleta tahara [usafi] kwa muumini, ndiomana Allah anaipenda, amesema Allah Mwenye Nguvu na Utukufu: {Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojitakasa} [Baqarah :222]

Amesema Mtume [s.a.w] «Usafi ni nusu ya imani»(Imepokewa na muslim)

Tohara [usafi] ni nusu ya imani, kwasababu ni aina moja muhimu ya imani, na Allah anapenda aina zote za tohara [usafi]basi iwe ni:

  1. Tohara ya maana isiyo onekana

Ambayo inakusudiwa kuitahirisha nafsi kutokana na athari za madhambi na maasi na kumshirikisha Allah, nayo ni kwa kutubia toba ya kikweli kweli , na kutahirisha moyo kutokana na uchafu wa shirki, na shaka, na hasadi, na chuki, na ugonvi, na kiburi, na mtu kujitahirisha kutokamana na vitu hivi haiwezikani mpaka ipatikane ikhlasi [kufanya vyote hivi kwa ajili ya Allah pekee], na kupenda kheri na upole na unyenyekevu na ukweli, na kufanya kwa kutaraji radhi za Allah kupitia vitendo hivi.

  1. Tohara [usafi] wakihisia unaoonekana

Unakusudiwa usafi huu kuondoa uchafu na hadadhi.

Kuondoa najisi na uchafu:

Inakuwa kwakuondoa najisi kwa kutumia maji masafi, nguoni au mwilini au sehemu utakayotekeleza ibada, na kila kinacho ingia chini ya hivi.

Kuondoa hadathi

Inakusudiwa hapa kutia udhu, na kuoga na kutayamam; kwa ajili ya kusali, au kusoma quran, au kutufu alqa’aba nyumba yake Allah, au kumtaja na kumkumbuka yeye Allah Mtukufu, ama aina nyebgine za ibada.

Amesema Mtume [s.a.w] ‘usafi ni nusu ya imani’ [imepokewa na Muslim]

SWALA

Kumpwekesha Allah kunadhihirika wazi katika sala ambayo ndio mawasiliano pekee baina ya mja na Mola wake, hapo ndipo mja anamuonyesha Mola wake jinsi gani anamtii na kumpenda na kunyenyekea kwake, kwahio sala ni nguzo kubwa katika nguzo za uisilamu baada ya shahada mbili, nayo ni nguzo ya dini na nuru ya yakini, ndani ya sala nafsi inatengezeka na kifua kukunjuka na moyo kutulia, sala ni kizuizi cha kufanya maovu na ni sababu ya kufutiwa makosa, nayo ni vitendo maalumu kwa wakati maalumu vinavyo funguliwa kwa takbir na kumalizwa kwa salamu.

Na mwenye kuacha sala kwa kuikanusha amempinga Allah na Mtume wake, na kukataa amri za quran, na haya yanaenda kinyume na asili ya imani, ama Yule anaye kubali kuwa ni lazima kusali lakini akaiacha kwa uvivu tu basi ameihatarisha nafsi yake kwa hatari kubwa na makemeo makali, amesema Mtume [s.a.w] «Tofauti ilioko baina ya muislamu na ushirikina na ukafiri ni kuacha sala»(Imepokewa na Muslimu)

Wamesema baadhi ya wanavyuoni kuwa ni ukafiri pia, lakini si ukafiri ule mkubwa unaomtoa mtu katika uislamu, lakini hata hivyo ni dhambi kubwa na ni moja wapo ya yale madhambi yenye kuangamiza.

Swala iko na athari kubwa sana miongoni mwazo:

Amesema Mtume[s.a.w] ‘Swala ni nuru’ [imepokewa na Albaihaqi]

  1. swala inazuia kutenda maovu na mabaya, amesema Allah Mtukufu: {.SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.} [AL-Ankabuut : 45]
  2. Aamali bora baada ya shahada mbili ni sala, kwa hadithi ya Abdullah Ibn Masuud [r.a] amesema: «Nilimuuliza Mtume wa Allah[s.a.w] ni a’amali gani bora zaidi? Akasema ni kusali kwa wakati wake, akasema: nikamuuliza tena ipi? Akasema: nikuwafanyia wema wazazi wawili, akasema: nikamuuliza tena ipi? Akasema: nikupigana jihadi kwa njia ya Allah» (Imepokewa na Muslim)

Ni amali bora ambayo mja anajikaribisha kwa Allah.

  1. Swala inayaosha madhambi madogo, kwahadithi ya Jaabir Ibn Abdillah[r.a] alisema: alisema Mtume wa Allah[s.a.w]: « Mfano wa sala tano ni mfano wa mto unaopita karibu na mlango wa nyumba ya mmoja wenu, naye anaoga katika mto huo mara tano kwa siku» (Imepokewa na Muslim)
  2. Sala ni nuru kwa mwenye kuisali hapa duniani na kesho akhera pia, amesema Mtume [s.a.w] kuhusu sala:«mwenye kuihifadhi sala itakuwa kwake nuru na mwangaza na utetezi siku ya kiyama, na asiye ihifadhi haitakuwa kwake nuru wala mwangaza na utetezi, na atakuwa siku ya kiyama pamoja na Firauni na Qaruni na Hamana na Ubai Bin Khalaf» (Imepokewa na muslim)

Akasema tena Mtume [s.a.w]« sala ni nuru» (Imepokewa na Albaihaqi)

  1. Swala inamuenua mtu daraja na kumfutia madhambi madogo, kwa hadiith ya Thaubani Maula wa Mtume [s.a.w] alimwambiya: «Juu yako kukithirisha sujudu, kwasababuu hautasujudu kwa ajili ya Allah hata sijda moja ila utanyenyuliwa daraja na kufutiwa madhambi kwayo»
    (Imepokewa na Muslim)
  2. Swala ni sababu kuu yakuingia peponi pamoja na Mtume[s.a.w] kwa hadiith ya Rabii’a Ibn Ka’ab Al-aslamiyu [r.a] alisema: «nilikuwa na lala pamoja na Mtume wa Allah [s.a.w] nikamletea maji atawadhe na kila alichokitaka akaniambia: omba lolote, nikamwambia:’ naomba kuwa pamoja nawe peponi,’ akaniambia huna lengine lakuomba? Nikamwambia hilohilo tu’ akaniambia: basi nisaidiye kwa kusujudu sana [kusali sana» (Imepokewa na Muslim)Ni mawasiliano ya moja kwa moja baina ya mja dhaifu na Mola wake Muweza aliye na nguvu na utukufu, na anakithirisha kumtaja Mola wake na kushikamana moyo wake naye, na hili ndilo lengo muhimu sana la sala, amesema Allah:{Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi}. [TA-HA : 14]      

 ZAKA 

Zaka ni kutahirisha na kukuza nafsi na mali na jamii,

Mtukufu: {Simamisha sala kwa kunitaja.} [Taha :14]

Katika kukuza na kutahirisha, usafi wa nafsi ya mja anayempwekesha Mola wake unamfanya atoe mali yake na kuisafisha kupitia zaka, kwani zaka ni haki ya lazima kutoka kwa matajiri kupatiwa mafakiri, na wanaofanana nao, kwalengo la kumridhisha Allah na kuitakasa nafsi na kutendea wema walio na haja.

Zaka iko na umuhimu sana katika uislamu, ndio maana likawa lengo la kuekwa zaka laonyesha umuhimu wake. Na atakae chunguza katika sababu za zaka ataona umuhimu wa nguzo hii tukufu na athari zake kubwa, miongoni mwa hizo athari:

  1. kuitakasa nafsi ya mja kutokana na uchafu wa uchoyo na uroho na shari zote na utamaa ,
  2. kuwaliwaza masikini na wanyonge na wasiokuwa na kitu kwa kuwatoshelezea haja zao.
  3. kueka maslahi ya kijamii ambayo ndani yake kuna mahitajio ya kimaisha ya wanadamu na raha zao.
  4. Kumaliza mrundiko wa mali kwa baadhi ya matajiri na wafanyibiashara pekee, ili mali isije ikawa sehemu finyo kwa watu maalumu ama isiwe mali niyenye kuzunguka baina ya matajiri peke yao.
  5. zaka inafanya jamii ya kiislamu kuwa kama familia moja, aliye na uwezo anamuhurumia asiye na uwezo, na tajiri anamuhurumia aliye na dhiki.
  6. zaka inaondoa yaliyomo nafsini miongoni mwa chuki na hasira dhidi ya matajiri, na kuwahusudu na kuwadhamiria mabaya kwa yale walioneemeshwa na Allah.
  7. zaka ni kizuizi kinachozuiya kutokea maovu ya kimali , kama wizi na kupora na kuvamia mali za watu,
  8. zaka inakuza mali na kuitakasa.

Yamekuja mambo haya kwenye maandishi, yanayoonyesha wazi ulazima wa kutoa zaka, na akaeka wazi Mtume [s.a.w] kuwa zaka ni miongoni mwa nguzo na misingi ya uislamu muhimu sana ambayo uislamu ulijengwa kwazo, ndio maana ikafanywa kuwa nguzo ya tatu katika nguzo za uislamu. Amesema Allah Mtukufu: {Na simamisheni sala [enyi mayahudi] na toeni zaka na inameni pamoja na wanaoinama [yaani kuweni waislam]} [Albaqarah :43]

Na akasema tena, Allah Mtukufu: {Na simamisheni sala na toeni zaka; na kheri mtakazozitanguliza, kwa ajili ya nafsi zenu, mtazikuta kwa mwenyezi mungu. Hakika mwenyezi mungu anayaona [yote]mnayoyafanya.}
[Al baqara : 110]

Na katika hadiith ya Jibril mashuhuri: «Uislamu ni kushuhudia kuwa hakuna wakuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wake, na kusimamisha sala na kutoa zaka na kufunga mwezi wa ramadhani na kuhiji nyumba kongwe [maka] kwa mwenye uwezo.» (Imepokewa na Muslim)

Amesema Mtume [s.a.w] «Umejengwa uislamu kwa mambo manne : kushudia ya kuwa hakuna wakuabudiwa ila Allah na Muhamad ni Mtume wa Allah na kusimamisha sala na kutoa zaka na kuhiji na kufunga mwezi wa ramadhani» (Imepokewa na Albukhari)

Maandishi haya na mfano wake yanaonyesha wazi kabisa kuwa zaka ni moja katika nguzo za kiislamu, na misingi yake mikubwa, ambayo haukamiliki uislamu isipokuwa hiyo.

FUNGA /SAUMU

Allah alifaradhisha funga na kuifanya kuwa moja ya nguzo za kiislamu, nayo ni kujizuiya na vivunja saumu kwa nia ya ibada kutokea kwa asubuhi hadi kuzama kwa jua. Amesema Allah Mtukufu: { Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.} [Albaqarah : 186]

Na kukitisha imani katika moyo wa mja na kumpwekesha Mola wake ni sababu ya kutekeleza aliyofaradhishiwa, kwa kufuata neno lake Allah Mtukufu: { Enyi mlioamini mumelazimishwa kufunga [saumu] kama walivyolazimiswa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha mungu} [Al baqarah 183]

Wanafurahia wenye kumpwekesha Allah kwa kufunga na kupatilizia katika hilo, amesema Allah katika hadiith qudsi: «kila aamali ya mja wangu ni yake isipokuwa saumu hiyo ni yangu na mimi ndiye nitailipa.» (Imepokewa na Albukhari)

Saumu ni chuo chakujenga imani katika nafsi .

Athari za saumu kwa mja ni nyingi sana miongoni mwazo:

  1. saumu ni siri baina ya mja na Mola wake inayodhihirika katika kumlindiza Allah kikwelikweli katika moyo wa muislamu, kwasababu haiwezikani hata kidogo kuingia riaa katika ibada yake, saumu inamfundisha muumini kulindizia Allah na kumuogopa, na hili ndio lengo kubwa na makusudio ya hali ya juu yanayovunja matamanio mengi ya watu.
  2. saumu inafundisha utaratibu wa umoja na kupenda uadilifu na usawa, inajenga huruma kwa waumini na kusikitikiana na tabia nzuri, kama inavyohifadhi jamii kutokana na shari nyingi na ufisadi.
  3. saumu inamfanya muislamu ahisi machungu ya nduguze waislamu , ili hisia hizo zimfanye awe mwenye kutoa na kuwafanyia wema mafakiri na masikini, ndio yawe mapenzi yakikwelikweli kwaa undugu wa kiislamu.
  4. Saumu ni mazoezi ya kujifunza kudhibiti nafsi na kuibebesha majukumu na kuibebesha mambo magumu na mashaka.
  5. saumu ni kinga inayomkinga mwandamu kufanya dhambi, inamlipa kheri nyingi, amesema Mtume [s.a.w] «Funga ni ngao , basi mmoja wenu anapo funga asijiropokee tu wala asijifanye mjinga, na kama mtu akimchokoza au kumtukana basi aseme : mimi nimefunga akarudia mara mbili. Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, hakika harufu inayotoka kwenye mdomo wa aliyefunga inanukia vizuri sana kwa Allah kuliko miski, kwasababu ya kuacha chakula chake na kinywaji chake na matamanio yake kwa ajili yangu, funga ni yangu mimi ndiye nitailipa, kila jema moma linathawabu kumi mfano wake.»(Imepokewa na Albukhari)

HAJJI

Kumpwekesha Allah kunadhihirika katika Hajj, Hajj nimiongoni mwa ibada ambazo zinamuongezea muilsamu tawhiid yake, na kujipamba na imani kamili; katika hajj mtu anatangaza tawhiid yake aingiapo hajj tu akisema: ”nimeitikia mwito ewe Mola wangu nimeitikia huna mshirika Mola wangu nimeitikia”. Si mwanzo wakuingia tu peke yake, bali katika kila sehemu na kila hatua anakariri maneno haya, ili arudi wakati wa kurudi akiwa amefutiwa madhambi yake yote, na kurudi kama siku aliyozaliwa na mamake, kwasababu ya tawhiid tu na kuitangaza, hajj ni kukusudia kwenda nyumba tukufu, katika masiku maalumu ya hajj, kwa nia ya kutekeleza ibada ya hajj, kama ilivyofudhishwa kutoka kwa Allah, na kama alivyo hiji Mtume [s.a.w] nayo ni faradhi kutoka kwake Allah kwa viumbe vyake, iliyothibiti kwa maandiko ya qurani na suna zake Mtume [s.a.w] na maafikiano ya waislamu wote.

Miongoni mwa athari za hajj kwa maisha ya mwanadamu:

Amesema Mtume [s.a.w] hakika imeekwa tawafu [kuzunguka alka’aba] na kuenda swafa na marwa , na kurusha vijiwe katika jamarat, kwa ajili ya kuendeleza kutaja jina lake Allah [imepokewa na Ahmed]

  1. 1-ni sababu ya kufutiwa dhambi na makosa amesema Mtume [s.a.w]«Kwani hukujua uislamu unayaporomosha yaliotangulia [kuyafuta madhambi] na hijra [kuama kwa ajili ya Allah] kuna poromosha yaliyo tangulia [futa madhambi] na hajj inaporomosha yaliyotangulia [futa madhambi]»
    (Imepokewa na Muslim.)
  2. Hajj nikutekeleza amri zake Allah, mtu anaacha watu wake, anamuacha mtoto wake, anavua nguo zake za kawaida, anatangaza tawhiid ya mola wake, yote haya nikutekeleza maamrisho ya Mola wake na haya ndio maamrisho mazito kweli kuyatekeleza.
  3. Hajj ni sababu ya kupata radhi za Allah na kuingia peponi , amesema Mtume [s.a.w]«Hajj ya kweli haina malipo ila pepo»(Mutafaqun ilaihi)
  4. Hajj ni kudhihirisha wazi wazi usawa na uadilifu kwa watu, wakati wanaposimama watu kisimamo kimoja kwenye uwanja wa Arafat, hakuna ubaguzi wa cheo cha kidunia isipokuwa kwa uchaji wao na kumpwekesha kwao Allah.
  5. katika Hajj kuna kukitisha misingi ya kujuana na kusaidiana, kujuana kunakua kwingi, na watu wanashauriana baina yao na kubadilishana mawazo, ambayo yatajalia kuendelea uma wa kiislamu na kuzidi kujiendeleza katika mambo ya uongozi na siyasa.
  6. Hajj inalingalia kwa tawhiid [kumpwekesha Allah] na ikhlas [kumtakasia Allah ibada] mambo ambayo ndiyo ataishi nayo katika umri wake wote baada ya hapo, hampwekeshi ila Allah wala hamuombi ispokuwa Allah pekee.