KHOFU

KHOFU

{Na Mwenyezi Mungu anakutahadharisheni na adhabu zake} [aali imran :30]

MAANA YAKE:

Khofu ya Allah ni miongoni mwa ibada za moyo zilizo kubwa, amesema Allah Mtukufu: {Hakika huyo ni Shet'ani anawatia khofu marafiki zake, basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi mkiwa nyinyi ni Waumini.} [Aali Imran : 175]

Katika aya hii kunaulazima wa kumuogopa Allah pekee. na kukokoteza kuwa kumuogopa Allah ni miongoni mwa misingi ya imani, na kadri imani ya mja itakuwa kubwa ndiyo khofu yake kwa Allah nayo inakuwa kubwa.

Kutoka kwa mama Aisha [r.a] amesema:«Nilimuuliza Mtume[s.a.w] kuhusu ayah hii» {Na hao ambao wanatoa [zaka na sadaka katika mali] waliyopewa, na hali nyoyo zao zinaogopa}«JE niwale wanao kunywa pombe na kuiba ? akasema : ” la! Ewe Binti wa As-Swidik, ni wale ambao wanafunga na wanaswali na wanatoa zaka nao wanaogopa zisijekutotakabaliwa aamali zao» (Imepokewa na Atirmidhi)

VITU VYENYE KULETA KHOFU YA ALLAH. 

  1. Kumtukuza Allah na kumuhishimu kwa kumtambua yeye na kuyatambua majina yake na sifa zake. {Wanamuogopa Mola wao Aliye juu yao} [An nahl : 50]
  2. Khofu ya Allah impelekee mtu kuogopa na kujikinga na vitu vyenye kuudhi vya adhabu kali motoni na marejeo yaliyo mabaya.
  3. Kuhisi kwake upungufu katika kutekeleza mambo ya lazima aliyo yalazimisha Allah, pamoja na kutambua kuwa Allah anamjua, na anamuona na anauwezo juu yake, bila kuangalia udogo wa kosa kwa mtizamo wake lakini ukubwa wa mwenye kukosewa.naye ni Allah.
  4. Kuzingatia maneno yake Allah yaliyojaa ahadi zake, kama kemeo la juu ya wanao muasi yeye na kukanusha sheria zake, na kuacha nuru ambayo walikuja nayo mitume[a.s]
  5. Kuzingatia maneno yake Allah na Mtume wake pamoja na kuangalia sera yake.
  6. Kutafakari ukubwa wa Allah Mtukufu, kwasababu mwenye kutafakari juu ya ukubwa wa Allah itampelekea kuzifahamu sifa zake Allah na ukubwa wake, na mtu yeyote ambaye moyo wake utakiri ukubwa wa Allah bila shaka mtu huyu atamuogopa Allah.

Amesema Allah Mtukufu: {Na Mwenyezi Mungu anakutahadharisheni na adhabu zake} [Aali Imran :28]

Akasema Allah Mtukufu: {Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri yake. Na Siku ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono wake wa kuume.} [Az-zumar : 67]

Khofu ya Allah inalazimu elimu ya kumtambua Allah, na elimu ya kumtambua Allah inalazimu kumkhofu , na kumkhofu Allah inalazimu kumtii.}

  1. Kuyafikiria mauti na ugumu wake, na kuwa hakuna njia ya kuyakimbia: {Sema,’hakika mauti haya mnayoyakimbia, bila shaka yatakutana nanyi; } [AL-JUMUA :8]

Hivi ndivyo inalazimu khofu ya Allah, amesema Mtume [s.a.w] «Kithirisheni sana kukumbuka kivunja ladha zote [mauti] kwasababu hakuna anayeyakumbuka awe katika maisha ya dhiki isipokuwa Allah atayakunjua, au awe katika maisha ya wasaa isipokuwa Allah atayadhiki» (Imepokewa na Atabarani)

  1. Kuyafikiria yatakayotokea baada ya mauti ndani ya kaburi na misukosuko yake. Amesema Mtume [s.a.w]«nilikuwa nimewakataza kuyazuru makaburi lakini sasa yazuruni, kwasababu huko kuyazuru kutamfanya mtu aipenyongo dunia na kuikumbuka akhera»
    (Imepokewa na Ibn Majah)

Na kutoka kwa Baraa [r.a] amesema: «Tulikuwa na Mtume [s.a.w] katika Jeneza, akakaa pembezoni mwa kaburi, kisha akalia paka mchanga ukalowana machozi, kisha akasema: “Enyi ndugu zangu mfano wa safari hii mjiandae nayo»
(Imepokewa na Ibn Majah)

Na amesema Allah Mtukufu: {Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana, wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi Mungu mdanganyifu.} [Luqman :33]

  1. Kutafakari mwisho wa madhambi madogo ambayo mwanadamu anayadharau, akayafananisha Mtume [s.a.w] na watu walio piga kambi katika jangwa kila mmoja wao akaleta kijiti mpaka wakavikusanya nakupikia mkate wao wazi vitaivisha mkate wao, kuna uhusiano baina ya vijiti na kuivisha mkate na baina ya madhambi yatakayo ivisha ngozi za mwanadamu. {Kila ngozi zao zikiiva tunawabadilishia ngozi zengine}

[An nisaa :56]

  1. Atambue mja kwamba anaweza kuzuiwa kufanya toba kwasababu ya kifo cha ghafla, na majuto hayatamfaa wakati huo. Amesema Allah Mtukufu: {Hata yanapomfika mmoja wao mauti, husema: mola wangu! Nirudishe [ulimwenguni]} [AL-muminun :99]

Aakasema tena : {Na waonye siku ya majuto} [Maryam :39]

  1. Kufikiria mwisho mbaya, amesema Allah Mtukufu: {Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao} [Al anfal : 50]
  2. Kukaa na watu ambao wanakuongezea uchaji Mungu na unyenyekevu kwake. Amesema Allah Mtukufu: {Na ujiweke pamoja na wale wanaomuabudu Mola wao asubuhi na jioni, hali ya kuwa wanataka radhi yake.}
    [Alkahf : 28]

KHOFU YA ALLAH INAAMBATANA NA KADHIA MBILI:

a-Kuogopa adhabu yake

Adhabu ambayo aliwaahidi wanaomshirikisha na kitu chochote na wale wanaomuasi na kujieka mbali na twaa yake.

b-Kumuogopa Allah:

Nayo ni khofu ya wanavuoni wanaomtambua Allah vizuri. {Na Mwenyezi Mungu anakutahadharisheni na adhabu yake,} [Aali Imran : 28]

Na kila mtu anapozidi kumtambua Allah huzidi kumcha, amesema Allah Mtukufu: {Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu [wanavyuoni]} [Fatir: 28]

Kwasababu walipo mtambua Allah kwa ukamilifu, kwa kuyajua majina yake na sifa zake, elimu hii ikazalisha khofu ya Allah, na athari zake zikaingia moyoni kisha zikadhihirika kwa vitendo.

Khofu itakapotulia kifuani mwa a.

MIONGONI MWA MATUNDA YA KHOFU YA ALLAH:

a-duniani:

  1. Ni miongoni mwa sababu za kumakinishwa ardhini na kuongezwa imani na utulivu; kwasababu ukipata unachoahidiwa tayari unapata uhakika zaidi: amesema Allah Mtukufu: {Na wale waliokufuru wakawaambia mitume yao: ”tutakutoeni katika nchi yetu au lazima murudi katika mila yetu.” Basi mola wao akawaletea wahyi kuwa “tutawaangamiza madhalimu”. Na tutakukalisheni [nyinyi] katika nchi [hizi] baada yao .”Watapata haya wale waliogopa maonyo yangu.}
    [Ibrahim: 13-14]
  2. Inahimiza kufanya matendo mazuri na kuwa na ikhlasi katika kutenda vitendo hivyo, bila kutaka malipo yakidunia yasijepungua malipo ya akhera, amesema Allah Mtukufu: {[Husema wenyewe katika nyoyo zao wanapowapa chakula hicho ] “ Tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu hatutaki kwenu malipo wala shukurani . Hakika sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu} [Al –insan : 9-10]

Akasema tena: {Katika Nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameamrisha zitukuzwe, na humo litajwe jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni * Watu

ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.} [An nur: 36-37]

Nyoyo zitadahadari na kuwa na wasiwasi na kuogopa, na khofu ya kuogopa siku hio ndio imewapelekea kutenda vitendo vyema, wakitaka kuepukana na shida hizo wakitahadhari maangamivu ya siku hio wakiechelea kupewa vitabu vyao kwa mikono yao yakushoto.

Khofu itakapo tulia kifuani mwa mtu huchoma matamanio yake na kufukuza kupenda dunia.

Mwenye kumuogopa Allah khofu yake itamwelekeza katika kila la kheri.

b-Akhera :

  1. Atakuwa mja chini ya kivuli cha Arshi siku ya kiyama, amesema Mtume [s.a.w]:«na mtu aliyetakiwa na mwanamke mwenye cheo na uzuri kufanya uchafu; akasema hakika mimi na muogopa Allah»(Imepokewa na Albukhar)

Dhahiri ya maneno haya yanatoka ulimini mwake kwa ajili ya kumuogopesha mwanamke huyo kutokamana na kitendo chake hicho cha kumtaka mtu huyo kwa uchafu, na kuikumbusha nafsi yake na kubaki katika msimamo wake huo bila kurudi nyuma baada ya maamuzi ya mwanzo. « na mtu aliyemtaja Allah akiwa pekee, mpaka machozi yakambubujika»
(Imepokewa na Albukhari)

Kuogopa Allah kunasababisha kutokwa na machozi, na macho yatakayo tokwa na machozi kwa ajili ya Allah basi hayataguswa na moto siku ya kiyama

  1. Ni sababu ya kusamehewa na Allah, na ushahidi wa maneno haya ni hadith yake Mtume[s.a.w] «Kulikuwa na mtu kabla yenu nyinyi Allah alimruzuku mali za kutosha, alipokaribia kufa akawaambia wanawe, ebu niambieni nilikuwa baba wa aina gani kwenu? wakasema: ”ulikuwa baba mzuri tu “akasema hakika mimi sijafanya memo yoyote, basi nikifa mnichome, kisha mnisage na mnieke mahala peupe siku ya upepo mkali, wakafanya kama walivyoelekezwa, lakini Allah Mwenye Nguvu na Utukufu akamkusanya na kumuuliza kwanini kafanya hivyo akajibu kuwa kafanya hivyo kwa kumuogopa Allah. Naye Allah akamsamehe na kumrehemu!!» (Imepokewa na Albukhari)

Allah akampatia udhuri kwa ujinga wake, na khofu yake kwa Allah ikawa ni sababu ya kusamehewa, [kwasababu kama angelikuwa na elimu asingepata msamaha] kwasababu dhahirri ya vitendo hivi nikuepa kufufuliwa, na tunajua kuwa yoyote atakaye pinga kufufuliwa ni kafiri.

  1. Inampeleka mwenye nayo peponi, kwasababu amesema Mtume[s.a.w] « Mwenye kuogopa huenda nyumbani mapema tena harakaharaka na mwenye kuenda mapema kwa harakaharaka bila shaka atafika nyumbani, sikilizeni, mjue kuwa bidhaa ya Allah iko ghali sana juweni kuwa bidhaa ya Allah ni pepo» (Imepokewa na Atirmidh)
  2. kuwa na amani siku ya kiyama,” amesema Allah katika hadiith qudsi : «Naapa na nguvu zangu siwezi kumkusanyia mja wangu khofu mbili au amani mbili, akinikhofu duniani nitampa amani akhera, na akiwa na amani duniani nitamtia khofu siku ya kiyama»(Imepokewa na Albaihaqi)
  3. Kuwa miongoni mwa waliosifiwa na Allah, mfano katika neno lake Allah: { Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na

wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.} [Al-ahzab : 35]

Yote haya ni maneno matakatifu yanayokusanya sifa za waumini.

Amesema Allah Mtukufu: { Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyo waruzuku}
[As-sajdah: 16]

Akasema tena: {Je! Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi...Sema: Ati watakuwa sawa wale wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.} [Az-zumar: 9]

Na akasema {Na ambao wanaiogopa adhabu [itokayo] kwa Mola. Hakika adhabu ya Mola wao si ya kusalimika nayo mtu [mbaya]} Al ma ‘arij: 27-28

Na Allah akawasifu waja wake walioko karibu zaidi, nao ni manabii, kwa khofu waliokuwanayo: {Bila shaka wao walikuwa wepesi wakufanya wema, na wakituomba kwa shauku na khofu.} [AL-ambiyaa :90]

Pia malaika wenyewe wanamuogopa Allah Mola wao, amesema Allah Mtukufu: {wanamuogopa Mola wao aliye juu yao, na wanatenda wanayoamrishwa.} [An nahl : 50]

  1. Kuridhiwa na Allah Mtukufu: {Mwenyezi mungu amewaridhia nao wameridhika. [malipo] hayo ni kwa yule anayemuogopa mola wake.}
    [Al- bayyinah:8]

Ni khofu ya wanaomtambua Allah 

Hakika wanaomtambua Allah ndivyo wanavyo mfanyia aamali na ndivyo wanavyo mtarajia , isipokuwa wanamuogopa Allah na wananyenyekea kwake sana katika sampuli zote za kunyenyekea. Kwa mfano:

Kulia kwake Mtume [s.a.w] akiwa anasali paka inasikika kutoka kifuani mwake sauti ya kwikwi, kama maji yachemkayo kwenye chungu. [Amepokea Ahmad, na Abuudauwd,na Annasaii]

Abubakar anashika ulimi wake huku akisema : «Huu ndio ulioniingiza katika maangamivu’ Huku akisema :‘ “laiti ningelikuwa mti wenyekuliwa na kuisha.» Umar Ibn khatab [r.a] anasema: «Laiti sikuwa chochote chenye kutajwa, laiti mamayangu hakunizaa»Anasema tena: «Kama ngamia aliyepotea atakufa huko kwenye mto wa Furat namimi ndio kiongozi wawaislamu ningeogopa kuulizwa na Allah siku ya kiyama»Na anasema: «Kama kutanadiwa mbinguni, kusemwe ‘enyi watu nyote mtaingia peponi ila mtu mmoja tu’ naogopa huyo mmoja anaweza kuwa mimi»

Uthman Ibn A’fan[r.a] amesema: «Ningependa nikifa nisifufuliwe»

Huyu ni Yule alikuwa akipitisha usiku mzima kwa kumsabihi Allah na kusali na kusoma Quran.

Mama wa waislamu Aisha [r.a] anasoma kauli yake Allah Mtukufu: {Basi Mwenyezi Mungu ametufanyia ihsani, [ametutia peponi] na ametuokoa na adhabu ya pepo moto} [At-tur :27]

Akiwa katika sala yake kisha akalia sana. {Ikiwa utawaadhibu, basi bila shaka hao ni waja wako; na ukiwasamehe basi kwa hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu na Mwenye hikima; [Al-maidah :118]

HUKUMU ZA KHOFU NA TANBIHI ZAKE

  1. [khashia ]kuogopa ina maana yajuu zaidi ya [khofu] kukhofia kwasababu khashia inapatikana kwa wale wanaomtambua zaidi Allah: {Kwahakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu [wanavyuoni]. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu ,Msamehevu} [Fatir : 28]

Khofu kwa Allah imeegemezwa na kumtambua Allah, amesema Mtume[s.a.w] « wallahi mimi nimcha Mungu zaidi kuwaliko na kumuogopa zaidi yenu» (Imepokewa na Muslim)

Kadri ya kumtambua Allah na kujua majina yake na sifa zake na ukamilifu wake na utukufu wake ndio kadri itakuwa khofu kwake na kumuogopa.

  1. khofu ya Allah inamanufaa kama itahimiza kujitahidi katika kufanya matendo mazuri na kutubia na kujuta na kuazimia kujivua katika maasi, kwahiyo khofi inachimbuka kwa kumtambua Allah, kwa kutambua ubaya wa kosa, na kusadikisha ahadi zake Allah, na kumjua Allah Mkubwa aliye juu, kwani hakuna khofu ambayo haimpelekei mtu kufanya vitendo vizuri na kujitahidi na kuleta toba.
  2. Khofu ya Allah ni jambo la lazima na nimiongoni mwa misingi ya imani, ni sehemu tukufu na njia iliyo na manufaa kwenye moyo wa mtu, nayo ni faradhi kwa kila mtu, inazuia mtu na maasi na kufuata dunia na marafiki waovu na inazuia na kughafilika na kutokuwa na hisia.

{Kwa hakika wanaomuogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu [wanavyuoni]. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu ,Msamehevu}[fatir : 28]

Mwenye kumuogopa Allah hakuna atakaye mdhuru, na mwenye kumuogopa asiye kuwa Allah hakuna atakaye mnufaisha.

Kutoka kwa Al-fudheil Ibn Iyaadh. 

Marejeo 

  1. Eleza na utaje vyenye kuongeza khofu yako kwa Allah Mtukufu.
  2. Taja majina ya Allah Matakatifu na sifa zake nzuri unazozifahamu zinazidisha khofu ya Allah kwako.
  3. Anaye mkhofu Allah anatakiwa afanye nini?